Tetesi za kujiuzulu Conte ni za uzushi - Aurelio De Laurentiis
Eric Buyanza
November 11, 2025
Share :

Rais wa Napoli Aurelio De Laurentiis amepuuza habari zilizoenea nchini Italia kwamba kocha wa Napoli, Antonio Conte anataka kujiuzulu wadhifa huo.
Uvumi huo uliibuka kufuatia Napoli kupata kipigo cha bao 2-0 dhidi ya Bologna mwishoni mwa wiki, huku taarifa zikienea kwamba kocha huyo alikuwa tayari kujiuzulu.
Akizungumzia suala hilo, De Laurentiis alisema taarifa hizo ni za uzushi.
"Ni hadithi ya uongo. Ninajivunia kuwa na mtu kama Conte karibu nami, yeye ni dhamana kwa klabu yetu, wachezaji na mashabiki."
Conte aliiongoza Napoli kutwaa taji la Serie A katika msimu wake wa kwanza klabuni hapo.
Hata hivyo, msimu huu, kikosi cha Conte kwa sasa kiko nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi ya Serie A, nyuma ya Roma, AC Milan na Inter Milan.





