TFF Yamfungia Shufaa Nyamlani kujihusisha na soka.
Joyce Shedrack
April 19, 2025
Share :
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limemfungia maisha Mtunza vifaa (Kit Manager) wa timu ya Taifa ya Beach Soccer na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Temeke (TEFA), Shufaa Jumanne Nyamlani kujihusisha na soka.
Nyamlani alishtakiwa na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kwa makosa matatu ambayo ni kuchochea Umma kwa ujumla kinyume na Kanuni ya 73(4) ya Kanuni za Maadili za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Toleo la Mwaka 2021, kutoheshimu uamuzi halali wa vyombo vya haki vya mpira wa miguu kinyume na Kanuni ya 73(8a) ya Kanuni za Maadili za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Toleo la 2021, na kutaka kuiondoa madarakani Kamati ya Utendaji ya Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Temeke (TEFA) kinyume na Kanuni ya 73(3a) ya Kanuni za Maadili za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Toleo la 2021.
Nyamlani alitumiwa wito ambao Kamati ilijiridhisha kuwa alipokea, lakini hakufika mbele ya Kamati bila kutoa taarifa yoyote.
Wito ulimhadharisha kwamba endapo asipotokea yeye au wawakilishi wake, shauri litasikilizwa bila uwepo wao (ex parte), Kamati iliendelea na shauri.
Baada ya kusikiliza malalamiko na ushahidi uliotolewa na kupitia nyaraka na vielelezo vilivyowasilishwa mbele yake, Kamati imemtia hatiani kwa makosa aliyoshtakiwa na imemfungia maisha kujihusisha na shughuli zote za mpira wa miguu ndani na nje ya Tanzania. Adhabu hiyo inaanza tarehe 16/04/2025.