Timu itakayofanya 'Ushirikina' uwanjani kukatwa pointi
Eric Buyanza
May 29, 2024
Share :
Bodi ya Ligi imesema kuelekea msimu ujao itatengeneza kanuni ya kuzikata pointi timu zitakazofanya au kuonyesha imani za kishirikina viwanjani wakati wa mchezo.
Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Steven Mguto, alisema wao kama bodi, Shirikisho la Soka Nchini (TFF) na wadau wengine wa soka, wanataka kutengeneza kanuni ya kuzikata pointi timu kutokana na kukithiri kwa vitendo hivyo msimu huu, akisema faini peke yake hazitoshi.
"Tutaweka sheria kali ambazo klabu zitaogopa na hazitafanya vitu kama hivi vya makusudi, moja ya sheria ni adhabu ya kunyang'anywa pointi, tukiweka hii watu watatia akili, hawatafanya mambo ya ovyo ovyo," alisema Mguto.
Amesema moja ya mambo yaliyowasumbua sana msimu huu ni matukio ya imani za kishirikina na wamezipiga sana faini klabu, lakini bado zinaonekana kutowaathiri wahusika.
"Wala isidhaniwe kuwa sisi tunapenda kuwapiga faini ili tupate fedha, sisi faini siyo bajeti yetu ya kujiendesha, lakini tunawajibika kufanya hivyo, naona bado haziwafundishi, tutakuja na sheria nyingine msimu ujao.
Sasa naona tukianza kuwakata pointi labda itasaidia kuondoa vitendo hivi," alisema Mguto.