Tour Guides ni kiungo muhimu kati ya vivutio vyetu vya utalii na wageni
Sisti Herman
July 28, 2025
Share :
Mwaka 2024, sekta ya utalii ilitajwa kuchangia zaidi ya asilimia 17.5 ya pato la Taifa ambapo vivutio vya utalii kama Hifadhi za Taifa za wanyamapori, milima, makumbusho huweza kuwavutia watalii wengi kuja kutalii nchini.
Waongoza watalii au 'Tour guides' kama wanavyofahamika zaidi wamekuwa kiungo muhimu cha mawasiliano kati ya Vivutio vyetu vya utalii na wageni ambao hutembelea na kupenda kufahamu mambo tofauti kuhusu vivutio vyetu, Tour guides huwapa ufahamu wa ndani zaidi.
Mbali na kuwapa ufahamu wa vivutio kwa kuwapa elimu kuhusu wanyama, simulizi za kihistoria, tamaduni hawa Tour Guides pia hupanga na kuongoza safari mbalimbali za watalii kwenye vivutio vyetu hali inayochangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa sekta ya utalii.
Je umewahi kujiuliza, ni vipi kama likitokea tatizo katikati ya safari hizi? Mfano gari kupata changamoto za kiufundi tena katikati ya Mbuga.

Basi Tour Guides hawa watakushangaza, PMTV imedodosa kuhusu hilo kwa kumhoji Alexandra Lieven De koker, mmoja kati ya mabinti wanaosoma kada hii kwenye chuo cha Professional Tour Guiding School ambaye anaeleza kuwa mbali na kuwa watu wamekariri kuwa kada yao inahusika na kuongoza watalii lakini pia wanafundishwa namna ya kukabiliana na changamoto za dharura kama hizo.

"Pindi gari kama Land Rover (ambazo mara nyingi hutumika kwenye Safari za Mbugani) ikipata changamoto katikati ya nyika kama Serengeti, tena changamoto kama ya tairi, kimya hutawala, hofu hutanda watalii wakihofia kuweza kukaa kwenye jua kali nyikani kama la Serengeti kumsubiri fundi, lakini kwasababu mimi kama muongoza njia nipo basi nakuwa na jukumu la kuweza kurekebisha haraka kwasababu tayari nilijifunza ufundi huo" anadokeza Alexandra.

Picha (juu & chini) humuonyesha Alexandra akiwa kwenye moja ya gereji Mianzini jijini Arusha wakati akiwa kwenye mafunzo kwa vitendo kwaajili ya kuongoza watalii.
Alexandra anaonyesha kuwa, Tour Guides ni zaidi ya kuongoza njia kwa watalii, bali ni kuwa fundi, mwalimu na kuna muda huweza kuwa hata mhudumu wa afya pindi inapohitajika huduma ya kwanza na kuwafanya watalii kutalii kwa usalama na amani kufurahia mapumziko yao.