Traore avunja uhusiano wa kidiplomasia na Ufaransa
Eric Buyanza
June 27, 2026
Share :

Serikali ya kijeshi ya Burkina Faso imetangaza rasmi jana Ijumaa (Juni 26, 2026), kwamba inavunja mahusiano yake ya kidiplomasia na Ufaransa.
Serikali hiyo chini ya Kapteni Ibrahim Traore ilitangaza uamuzi huo kupitia televisheni ya taifa (RTB). Hatua hiyo imehitimisha uhusiano rasmi wa kiserikali kati ya nchi hiyo na Ufaransa ambayo ilikuwa mtawala wake wa zamani wa kikoloni
Waziri wa Mawasiliano wa Burkina Faso, Gilbert Ouedraogo, alieleza kuwa nchi hiyo imechukua hatua hiyo baada ya kufanya tathmini ya kina na kubaini kuwa hakuna tena misingi ya kuheshimiana, kuaminiana, na kutoingiliana katika masuala ya ndani ya nchi.
Serikali ya Burkina Faso imeituhumu Ufaransa kwa kuwa na sera za 'ukoloni mamboleo' na kufadhili mitandao ya uasi pamoja na vikundi vya kigaidi vinavyosababisha vifo na machafuko katika ukanda wa Sahel. Ufaransa imewahi kukanusha tuhuma hizo huko nyuma na kuutaja uamuzi huo kuwa wa kiadui na usio na msingi.
Tangu mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2022, Burkina Faso imekuwa ikipunguza utegemezi wake kwa nchi za Magharibi. Badala yake, imeanza kujenga ushirikiano mpya wa kiusalama na nchi nyingine kama vile Urusi.





