Traoré azuiliwe ili kulinda maslahi ya kimataifa - Langley
Eric Buyanza
April 25, 2025
Share :
Katika hali isiyo ya kawaida, jina la Kapteni Ibrahim Traoré, kiongozi kijana wa Burkina Faso anayejitambulisha kama mpigania haki za Waafrika, limeingia katika vichwa vya habari vya dunia si kwa mapinduzi aliyoyafanya tu, bali kwa kile kinachotajwa kuwa ni shinikizo kutoka kwa Marekani kutaka akamatwe.
Tuhuma hizi hazijatolewa na mtu wa kawaida, bali ni kutoka kwa Jenerali wa nyota nne wa Marekani, Michael E. Langley, ambaye ni Kamanda wa Kikosi cha Marekani cha Afrika kinachoitwa United States Africa Command (AFRICOM).
Katika kikao rasmi cha Baraza la Seneti la Marekani wiki hii, Langley aliitwa kutoa tathmini kuhusu hali ya usalama barani Afrika. Katika maelezo yake, alimtaja wazi Kapteni Traoré, akisema kwamba anatumia dhahabu ya taifa lake "kujilinda binafsi" badala ya kuwalinda wananchi, na akaongeza kuwa kuna haja ya kumchukulia hatua kali za kimataifa, akisema:
"Tunapendekeza hatua mahususi, vikwazo vya kifedha, ushirikiano wa kimataifa, na ikiwa itahitajika, Traoré azuiliwe ili kulinda maslahi ya kikanda na kimataifa."
Kauli hiyo imetafsiriwa na wengi kuwa ni wito wa wazi wa kumkamata kiongozi huyo. Lakini je, kweli Traoré ni tishio kwa usalama wa dunia, au ni kiongozi asiyejiweka chini ya amri ya mataifa ya Magharibi?
Jenerali Michael E. Langley aliteuliwa mwezi Juni 2022 kushika wadhifa wa Kamanda wa AFRICOM, uteuzi uliothibitishwa na Baraza la Seneti mnamo Agosti 6, 2022. Kwa uteuzi huo, Langley aliingia kwenye historia kama Mmarekani Mweusi wa kwanza kufikia hadhi ya Jenerali wa nyota nne (Four-Star General) katika Jeshi la Wanamaji la Marekani, tangu kuanzishwa kwake miaka 246 iliyopita.
Cheo cha Jenerali wa nyota nne ni miongoni mwa vyeo vya juu kabisa katika safu ya kijeshi nchini Marekani. Kinampa mamlaka ya kutoa maamuzi ya kimkakati kuhusu operesheni za kijeshi duniani, hasa katika bara la Afrika ambako AFRICOM inaendesha shughuli za kijeshi na za ujasusi katika zaidi ya nchi 50.
Licha ya hadhi hiyo, Langley sasa anakabiliwa na maswali ya kiitikadi, hasa miongoni mwa Waafrika wanaomwona kama msaliti wa asili yake, anayesimamia maslahi ya kibeberu dhidi ya mustakabali wa bara lake la asili.
BBC