Treni 3 za SGR zakwama baada ya hitilafu ya Umeme
Sisti Herman
December 4, 2024
Share :
Shirika la Reli Tanzania TRC linauarifu umma kuhusu kusimama ghafla kwa treni za mwendokasi zilizokuwa zinasafiri kati ya Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma, kufuatia hitilafu ya umeme katika mifumo ya Gridi ya Taifa, kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Usambazaji Umeme Nchini TANESCO.
Hitilafu hiyo iliyotokea leo Disemba 04, 2024 majira ya saa 4.03 asubuhi, ilisababisha mikoa yote inayopata umeme katika Gridi ya Taifa kukosa umeme.
Abiria walioathirika kufuatia hitilafu hiyo ya umeme, ni wale walioanza safari yao saa 2.00 kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, abiria wa treni ya saa 3.30 kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma na abiria waliotoka na treni ya saa 3.50 kutoka Morogoro kwenda Dar es Salaam.
Kufuatia jitihada zilizofanyika, umeme ulirejea saa 5.30 asubuhi na safari kurejea kama kawaida. Shirika linawaomba radhi abiria kwa usumbufu uliojitokeza.
Aidha, Shirika linawashukuru abiria kwa uvumilivu wakati wa changamoto hiyo.