Treni yasafiri Kilomita 70 bila Dereva
Eric Buyanza
February 26, 2024
Share :
Shirika la Reli la India limeamuru uchunguzi ufanyike baada ya treni ya mizigo kusafiri zaidi ya kilomita 70 bila ya madereva.
Video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinaionyesha treni hiyo ikipita stesheni kadhaa ikiwa kwenye mwendo wa kasi.
Taarifa zinasema treni hiyo ilisafiri bila dereva siku ya Jumapili, na baadae maafisa wa shirika hilo walifanikiwa kuisimamisha bila kuleta madhara yoyote kwa raia na mali.
Treni hiyo iliyokuwa inavuta mabehewa 53, ilikuwa imebeba mawe na ilikuwa ikielekea Punjab kutoka Jammu.
Maafisa wanasema ilianza kushuka kwenye mteremko kwenye njia za reli baada ya dereva wa treni na msaidizi wake kushuka.
Treni hiyo ilikimbia kwa kasi ya karibu 100km/h na kufanikiwa kuvuka stesheni tano kabla ya kusimamishwa.