Tuachieni ngoma ya uchaguzi tuicheze na ccm kama Simba na Yanga - Mbowe
Eric Buyanza
June 25, 2024
Share :
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema Watanzania wanachopaswa kutambua na kukiweka akilini kuelekea Uchaguzi Mkuu mwakani ni kwamba, mpambano utakuwa ni wao na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Aidha, amewataka askari wa Jeshi la Polisi, kuacha mpambano huo uchezwe kama mechi ya Simba na Yanga kwa kusimamia kiapo chao cha kulinda raia na mali zao, kwa kuwa mali za raia nyingine ni pamoja na kura zao.
Mbowe ameitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na wananchi wa Waso, Tarafa ya Loliondo, Wilaya ya Ngorongoro jijini Arusha.
“CCM hakitaki hoja ya Katiba mpya na Tume Huru ya Uchaguzi, hawataki kwa sababu wanajua wakienda kwenye uchaguzi ulio huru na wa haki, watawatandika asubuhi misa ya kwanza.
“Tumewaambia wenzetu tunataka Tume Huru ya Uchaguzi, tunataka Katiba Mpya ili uchaguzi wetu uwe huru na haki, hawataki.
“Nimeona askari polisi hapa, niwaambie ndugu zangu wa polisi, mateso wanayoyapata Watanzania wote ni pamoja na ninyi. Na mateso haya yanasababishwa na CCM. Acheni kuwa machawa wa CCM, acheni kuwasaidia CCM. Simamieni haki katika nchi yetu,” amesema.
Amewaeleza askari polisi kwamba, wamekula kiapo cha kulinda raia na mali zao, hivyo mali za raia ni pamoja na kura zao.
“Askari wetu simamieni kiapo chenu, msiwe mawakala wa kuisaidia CCM. Tuachieni hiyo ngoma tucheze nao kama Simba na Yanga,” amesema Mbowe.
NIPASHE