Tukemee pepo la kuwashindanisha wasanii – Khadija Kopa
Eric Buyanza
September 6, 2025
Share :
Mwanamuziki mkongwe wa muziki wa Taarab, Khadija Kopa amesema mashabiki ni watu muhimu kwa wasanii ila wanaoweza kumnyanyua au kumshusha wakikukataa.
Kopa alisema ili msanii ukubalike, ni lazima mashabiki wasikilize ngoma zako na kuzielewa, watazipenda, watakupenda lakini ukizingua tu kidogo ni hao hao wanaoweza kukumaliza kisanaa.
Amesema shabiki wa kweli huwa anafurahia mafanikio ya msanii hata kama hayamnufaishi, ila tatizo baadhi yao hutaka kulinganisha wasanii.
Nasema haya kwa sababu nimeshuhudia sana. Shabiki unapomsapoti msanii wako, hakikisha unaheshimu na wengine. Siyo unamsifia mmoja na kumponda mwingine.
Hii inasababisha mashabiki wengine kumchukia hata kama hawakuwa na chuki naye.
"Mfano shabiki wa WCB haipendi Konde Gang kwa sababu ya matusi ya mashabiki wao, au shabiki wa Zuchu hampendi Nandy au Mimi na Mwanahawa Ally. Hii siyo sahihi, inatakiwa tukemee pepo la kuwashindanisha wasanii na tujenge pamoja ili tufike mbali," amesema Kopa ambaye ni mama mzazi wa msanii Zuchu.
Ameongeza: "Mabeef yanatengenezwa na mashabiki, huwa wanafanya wasanii wao wachukiwe bila sababu, kwa nini ulinganishe wasanii? Kwa nini umtafute bora kati yao na kwa nini usiwatengeneze wote kuwa bora, kiufupi baadhi ya mashabiki anamuua msanii wake."
MWANASPOTI