Tunamuonea Okello, tuamuonea sana
Eric Buyanza
May 14, 2026
Share :

Aliwahi kuniambia rafiki yangu mmoja kuwa Derby ya Simba na Yanga ndio Derby pekee inayochezwa kila siku katika uso wa dunia. Nilishangaa. Akaniambia nishushe glasi katika meza anifafanulie. Tulikuwa katika vikao vyetu vya kila wikiendi mahala fulani Jijini Dar es Salaam.
Aliniambia kando ya mechi za timu hizo ndani ya uwanja, nje ya uwanja kuna mechi nyingine nyingi. Kuna Derby ya mashabiki kupigana vijembe. Hii inachezwa katika vijiwe vyao kila siku.
Katika vijiwe hivyo umeibuka mjadala mpya wa nani kiungo bora wa ushambuliaji. Simba wanamtaja Clatous Chama. Yanga wanamtaja Allan Okello.
Bwamdogo Okello anapiga namba za kutosha. Anafunga. Ana Asisst. Anafanya vitu vitokee ndani ya timu. Yanga wamezibeba namba zake na kuja nazo kijiweni kubishana. Utamu uko hapa.
Simba hawako nyuma na mkongwe wao Chama. Kiwango chake kinawapa kiburi cha kubishana na Yanga . Hivi karibuni amewafunga Yanga bao la kideoni. Moja ya kero zinazochukiwa na manazi wa Yanga ni lile bao.
Lakini kumlimganisha Chama na Okello ni kumdogosha Chama na kumuonea Okello. Katika mpira wa Tanzania Chama ameshafanya kila kitu. Huu ni mjadala mfu tunaopaswa kuuacha haraka.
Bwamdogo Okello ana safari ndefu. Ana mengi ya kufanya ili tumuweke meza moja na Chama, lakini kwa sasa ni mapema kumlinganisha. Katika mechi mbili za hivi karibuni zilizowakutanisha Chama na Okello kiwanjani, Chama alikuwa katika kiwango bora.
Mechi moja iliyochezwa Unguja Chama alisababisha penati iliyopigwa na kuipa Simba ushindi. Mechi nyingine iliyochezwa pale Mbweni, Chama alilfunga bao la kideo na kupata tuzo ya Man of the Match.
Mechi zote hizi mbili Okello alikuwepo na hakuna alilofanya. Tumuache Chama. Uzuri wa Okello bado kijana mdogo. Ana muda mrefu wa kufanya makubwa na kuijenga career yake. Anao mlango wa kuufungua na kukua zaidi.
Katika ukuaji wake ajitahidi kufanya mambo makubwa katika mechi kubwa. Mchezaji mkubwa hujipambanua katika mechi kubwa. Kwa Okello alifanyie kazi hili.
Katika muda huu ambao ushindani wa Chama na Okello umezidi kushika kasi, nafikiri tumwambie ukweli kijana acheze tu soka lake. Ukweli huu utamsaidia na kukua zaidi, kuliko kumlinganisha na Chama.
@abdulmkeyenge1





