UBAYA UBWELA: Simba yarudisha tena majeshi kwa Mpanzu
Eric Buyanza
July 27, 2024
Share :
Klabu ya Simba imerudi tena kwenye meza ya mazungumzo na winga raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Elie Mpanzu, baada ya hapo awali kushindikana.
Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema viongozi wa Simba wameamua kurejea kwa nguvu zote baada ya kutoweka kwa mchezaji wao, Kibu Denis, anayedaiwa kutorokea nchini Norway, bila ruhusa ya waajiri wake.
Chanzo kinasema awali Simba ilipeleka ofa ya dola za Kimarekani 150,000 huku klabu yake ya AS Vita ikitaka dola 250,000 lakini sasa wekundu hao wameongeza pesa kufikia dola 200,000 kumchukua winga huyo.
"Kwa sasa viongozi wanahaha kwa sababu upande wa kushoto kuna Jushua Mutale, kulia alikuwa anategemewa zaidi Kibu, kwa haya yaliyotokea ni kwamba hata akirejea hatoweza kuwa sehemu ya kikosi, hivyo wameamua kurudi sokoni kusaka winga mwingine wa kulia mwenye kiwango cha kimataifa," kilisema chanzo cha taarifa hiyo.
Chanzo kingine kilisema mara hii ya pili mambo yana kwenda vizuri na huenda kuanzia leo Jumamosi anaweza kutangazwa rasmi kuwa mchezaji mpya wa Simba.
NIPASHE