Udi unaweza sababisha matatizo ya afya kwa baadhi ya watu
Eric Buyanza
July 6, 2026
Share :

Tafiti mbalimbali za kisayansi zinaonya kwamba moshi na harufu ya udi vinaweza kusababisha matatizo ya kiafya kwa watu wengi.
Katika video ya hivi karibuni aliyoichapisha kwenye Instagram, daktari wa magonjwa ya mapafu, Sonia Goyal, alieleza madhara ya kuvuta moshi wa udi kila siku.
Aliufananisha udi na sumu inayoingia polepole kwenye mapafu, akisema kuwa vichafuzi vinavyojitokeza kutokana na udi hutokana na mchakato wa kufukiza na vina madhara yanayofanana na yale ya kuvuta sigara.
Chuo cha Marekani cha Mzio, Pumu na Kinga (ACAAI) kilionya katika mkutano wake wa kisayansi uliofanyika Boston mwaka jana kwamba kuvuta moshi wa udi kunaweza kuwa hatari kwa watu wenye mzio na pumu, na pia kwa watoto na wazee. Chuo hicho kina makao yake Illinois na kina zaidi ya wataalamu 6,000 wa afya.
Kwa mujibu wa ripoti yao, kuvuta moshi wa udi kunaweza kusababisha maumivu ya kichwa, kupungua kwa ufanisi wa mfumo wa upumuaji, matatizo ya ngozi na mwitikio wa mzio.
Pia ilibainika kuwa kila gramu ya udi unaowaka hutoa takriban miligramu 45 za chembechembe (PM), ilhali sigara hutoa miligramu 10 tu. Hivyo, udi huzalisha chembechembe karibu mara nne zaidi ya sigara.
Pia, utafiti uliotajwa na Maktaba ya Kitaifa ya Tiba uligundua kuwa moshi wa vijiti vya udi unaweza kuongeza vifo vinavyotokana na magonjwa ya moyo na kiharusi kwa takriban asilimia 12.
"Watu wengi hawatambui kuwa udi unaweza kusababisha madhara, hasa kwa Watoto", anasema Mary Lee-Wang, mtaalamu wa 'allergy' na mwandishi mkuu wa utafiti huo.
BBC





