Ugomvi wa wazazi wasababisha kifo cha mtoto wa miezi 5
Eric Buyanza
January 13, 2024
Share :
Jeshi la Polisi mkoani Geita linamsaka Kabilu Mayege, mkazi wa Mtaa wa Kilimahewa Wilaya ya Geita kwa tuhuma za kumuua mtoto wake mwenye umri wa miezi mitano kwa kumpiga na mkanda na kiatu cha kike kisa kikidaiwa kuwa ni ugomvi wa kifamilia
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP), Safia Jongo amethibitisha tukio hilo na akieleza lilitokea Januari 11, 2024 majira ya saa saba usiku eneo lijulikanalo kama Kigamboni.
Kamanda Jongo amemtaja mtoto ambaye kwa sasa ni marehemu ni, Leonard Kubilu mwenye umri wa miezi mitano ambapo alifariki baada ya kupigwa kwa kutumia kiatu cha kike na mkanda na baba mzazi.
“Chanzo cha tukio hili ni ugomvi wa kifamilia na huyu baba alitoweka mara tu baada ya kufanya tukio hili lakini juhudi zinafanyika za kumtafuta mtuhumiwa.
“Kutokana na tukio hili nitoe wito kwa jamii kumrudia Mungu kwa sababu nikiangalia tukio kama hili hata kama kuna ugomvi, mtoto wa miezi mitano hajui hata kuongea alimkosea nini huyu baba.
“Kwa hiyo kama ni ugomvi kati ya mama na baba, sasa inakuaje ugomvi wa baba na mama unapelekea machungu kwa mtoto, mtoto anahusika na nini.” Ameshangaa Kamanda Jongo.