Ukraine yaituhumu Marekani kuisaidia Urusi
Eric Buyanza
October 15, 2026
Share :

Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Ukraine na Marekani umeingia kwenye mgogoro mkubwa baada ya serikali ya Kyiv kuishutumu waziwazi serikali ya Washington kwa kile ilichokiita "kuisaidia Urusi kinyume chake" kufuatia mfululizo wa mashambulizi makali ya makombora yaliyoukumba mji mkuu wa Kyiv.
Shutuma hizo zimekuja baada ya mji wa Kyiv kupigwa na makombora ya Urusi kwa siku mbili mfululizo. Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, ameeleza kuwa hatua ya washirika wao kuzuia au kuchelewesha taarifa za intelijensia kuhusu marushio ya makombora ya Urusi ni jambo "lisilokubalika kabisa na lisilo la haki".
Mbali na swala la intelijensia, maafisa wa ulinzi wa Ukraine wameeleza kuwa Marekani inahusika na hujuma dhidi ya mifumo yao ya mawasiliano ya kijeshi. Inadaiwa kuwa kasi ya mtandao wa satelaiti wa Starlink (chapa ya kijeshi ya Starshield) inayomilikiwa na bilionea Elon Musk imepunguzwa kwa makusudi, hatua ambayo imelemaza uwezo wa jeshi la Ukraine kuongoza droni za kivita dhidi ya maeneo yanayokaliwa na Urusi.
Akijibu malalamiko hayo, Elon Musk alifafanua kupitia mtandao wake wa kijamii kuwa udhibiti na maamuzi yote ya kuzuia kasi au matumizi ya mfumo huo yanashikiliwa kikamilifu na jeshi la Marekani pamoja na Ikulu ya White House, na si kampuni yake ya SpaceX.





