Urusi imetumia kombora la Korea kaskazini - Zelensky
Eric Buyanza
July 31, 2026
Share :

Zelensky amesema Urusi imetumia kombora la masafa marefu la Korea Kaskazini kwa mara ya kwanza katika shambulio lake la anga, lililolenga nyumba ya familia moja katika kijiji cha Radushne karibu na mji wa Kryvyi Rih.
Katika hotuba yake kwa njia ya video, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema uchunguzi utafanyika kuthibitisha taarifa hizo, ingawa kwa mujibu wa taarifa walizo nazo kwa sasa, kombora lililotumika linaaminika kuwa la Korea Kaskazini.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, watu sita wa familia moja waliuawa katika shambulio hilo la Radushne. Watu 10 walikuwa wakiishi katika nyumba hiyo, ambayo iliharibiwa kabisa.
Zelensky ameishutumu Urusi kwa kushirikiana na kile alichokiita "utawala wa kichaa wa Korea Kaskazini" ili kupata silaha na wanajeshi.
Urusi na Korea Kaskazini, taifa la kikomunisti lililojitenga na mataifa mengine, zimekubaliana kuimarisha ushirikiano wa kijeshi, ikiwemo kusaidiana wakati wa mahitaji.
Wanajeshi wa Korea Kaskazini walitumwa nchini Urusi mwaka 2024 na 2025 kusaidia katika mapambano dhidi ya majeshi ya Ukraine yaliyokuwa yamevuka mpaka na kuingia katika eneo la Kursk, magharibi mwa Urusi.
Kwa mujibu wa idara za ujasusi za Ukraine na mataifa ya Magharibi, Korea Kaskazini pia imeiuzia Urusi makombora ya masafa marefu, mizinga, mifumo ya kurusha roketi na risasi.
Ukraine imeonya kuwa Korea Kaskazini huenda ikatuma tena maelfu ya wanajeshi kuisaidia Urusi katika vita vinavyoendelea.





