Urusi kujenga mitambo ya Nyuklia Uganda
Sisti Herman
November 2, 2026
Share :

Russia imeanza mazungumzo na Uganda, Ghana, Ethiopia na Misri kuhusu uwezekano wa kujenga mitambo mikubwa ya kuzalisha umeme kwa kutumia nishati ya nyuklia, hatua inayolenga kuimarisha ushirikiano wa nishati kati ya nchi hiyo na Afrika.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Serikali la Nishati ya Nyuklia la Russia (Rosatom), Alexei Likhachev, amesema nchi hiyo ipo tayari kushirikiana na mataifa ya Afrika kuanzisha mitambo ya nyuklia yenye ukubwa na mifumo tofauti, kulingana na mahitaji ya kila nchi.
Akizungumza Oktoba 31,2026 Likhachev alisema ushirikiano huo hautafungamanishwa na mradi mmoja wa aina moja, bali utazingatia mazingira, mahitaji na vipaumbele vya kila nchi.
“Ushirikiano wetu umejengwa katika msingi kwamba Afrika ina nchi zenye mahitaji na mazingira tofauti. Kwa hiyo, tunafuata mkakati maalumu kwa kila nchi, ambao hauishii katika mradi mmoja pekee,” alisema.
Ushirikiano wa nishati ya nyuklia ulikuwa miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa katika mkutano wa Russia na Afrika uliofanyika mjini Moscow wiki iliyopita.
Mkutano huo uliwakutanisha wawakilishi kutoka takribani nchi 50 za Afrika, wakiwemo wakuu wa nchi na serikali.





