pmbet

Urusi yadungua drone 600 zilizoelekezwa Moscow

Sisti Herman

November 16, 2026
Share :

 

 

Jeshi la Urusi limesema limefanikiwa kudungua takribani droni 600 zilizokuwa zikielekea katika mji mkuu wa nchi hiyo, Moscow katika mashambulizi ya usiku kucha hadi Jumatatu asubuhi, siku chache kabla ya Rais Vladimir Putin kukutana na Rais wa Marekani Donald Trump na Rais wa China Xi Jinping.

Meya wa Moscow, Sergey Sobyanin amesema mifumo ya ulinzi wa anga ya Urusi ilifanikiwa kuzuia droni hizo, huku 191 kati yake zikidhibitiwa wakati zikikaribia mji wa Moscow. Hata hivyo, hadi sasa hakuna taarifa rasmi kuhusu kiwango cha uharibifu au idadi ya watu waliojeruhiwa au kufariki dunia.

Mashambulizi hayo yametokea saa chache baada ya vikosi vya Ukraine kushambulia kiwanda kikubwa cha kemikali za petroli, kiwanda cha kusafisha mafuta na eneo la uzalishaji wa zana za kijeshi nchini Urusi, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Kyiv wa kushambulia maeneo muhimu ndani ya ardhi ya Urusi.

Wakati hali hiyo ikiendelea, China imethibitisha kuwa Xi Jinping atakutana na Trump na Putin Novemba 19 mjini Shenzhen, pembezoni mwa mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi Asia na Pasifiki (APEC). Hata hivyo, maafisa wa Marekani wamesema vita vya Urusi dhidi ya Ukraine havitarajiwi kujadiliwa katika mazungumzo hayo ya pande tatu.

Badala yake, Marekani inaendelea na mazungumzo tofauti yanayohusisha Kyiv na Moscow kwa lengo la kutafuta suluhu ya vita hivyo. Mazungumzo hayo yanafanyika wakati mvutano kuhusu nafasi ya Ukraine katika maamuzi ya kimataifa ukiendelea kuibua mjadala.

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, ameonya kuwa mkutano wa Shenzhen unaweza kufanana na Mkutano wa Yalta wa mwaka 1945, ambapo mataifa makubwa yalifanya maamuzi kuhusu maeneo ya ushawishi bila kuwashirikisha kikamilifu nchi ndogo zilizoathiriwa na maamuzi hayo.
 

pmbet
pmbet

Leagues standings

Tanzania Premier League
pmbet
pmbet