USA yapendelewa kujenga kambi zake za kijeshi Somaliland
Sisti Herman
February 23, 2026
Share :

Serikali ya Somaliland imetangaza kuwa ipo tayari kuipa Marekani upendeleo maalumu wa kupata madini adimu pamoja na fursa ya kujenga kambi za kijeshi katika eneo lake, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kiusalama na mataifa yenye ushawishi duniani.
Hatua hiyo imekuja wakati Somaliland, iliyojitenga na Somalia tangu mwaka 1991, ikiendeleza juhudi za kutafuta kutambuliwa rasmi kama taifa huru katika jumuiya ya kimataifa.
Akizungumza jana Jumapili Februari 22, 2026, Waziri wa Ofisi ya Rais wa Somaliland, Khadar Hussein Abdi, ameliambia Shirika la Habari la AFP kuwa mamlaka za Hargeisa zipo tayari kutoa haki za kipekee kwa Marekani katika sekta ya madini, na pia maeneo ya kimkakati kwa ajili ya kambi za kijeshi.
“Tumeweka wazi kuwa tupo tayari kuwapa Marekani haki ya pekee ya kupata madini yetu. Pia tupo tayari kutoa maeneo kwa ajili ya kambi za kijeshi. Tunaamini tutafikia mwafaka,” amesema Abdi katika mahojiano hayo.
Kwa mujibu wa kauli za viongozi wa Somaliland, hatua hiyo inalenga kuvutia uwekezaji wa kimkakati na ulinzi kutoka mataifa washirika, hasa katika kipindi ambacho eneo hilo linazidisha kampeni za kidiplomasia za kutambuliwa kimataifa.
Hata hivyo, licha ya kuwa na pasipoti, sarafu, jeshi na taasisi zake za dola tangu 1991, Serikali ya Mogadishu bado inachukulia Somaliland kuwa sehemu ya himaya ya Somalia.





