pmbet

Usisukutue mdomo na maji baada ya kupiga mswaki - Daktari

Eric Buyanza

April 27, 2026
Share :

Wizara ya Afya, imesema kuwa mara baada ya kumaliza kupiga mswaki kinywa na meno, mtu hatakiwi kusukutua mdomo kwa kutumia maji au kimiminika chochote kile, ili kuongeza ufanisi dawa ya meno.
 

Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Kinywa na Meno, Wizara ya Afya, Dk. Baraka Nzobo, amesema hayo akizungumza na NipasheDigital, kwa lengo la kutoa elimu.
 

“Nafahamu ni ngumu sana watu kuamini na kuacha tabia hii ya kusukutua na maji mara baada ya kumaliza kupiga mswaki meno kwani toka wamezaliwa mpaka wanafika umri wa utu uzima wamekuwa wakifanya hivyo.
 

“Lakini hawana budi sasa kuanza taratibu kuzoea kanuni hii ya kulinda meno kwa kutumia njia ya kupiga mswaki kwa kutumia dawa ya meno yenye madini ya fluoride. 
 

“Ukisukutua na maji kuondoa mapovu ya dawa  ya meno baada ya kupiga mswaki unakuwa haujafanya  chochote kulinda meno yako.”
 

Amesema sababu ya kutotakiwa kusukutua baada ya kumaliza kupiga mswaki meno na dawa ya meno yenye madini ya fluoride, kwa husababisha kuondoa madini hayo, yanayotakiwa kubaki mdomoni yakizunguka kwenye mate kulinda meno yako. 
 

Amesema mtu anapomaliza kupiga mswaki anashauriwa kutema mapovu yote na kutosukutua ili kuiacha fluoride kubaki ikizunguka kwenye mate na kusaidia kuyalinda meno yasitoboke.

 

“Fluoride iliyopo kwenye dawa za meno inapobaki mdomoni baada ya kupiga mswaki huchanganyika na mate na hivyo kusaidia kuvuta madini ya calsiam na phosphate.
 

“Kwa pamoja vikiungana na fluoride hutengeneza utando mgumu kwenye gamba la nje la jino (fluorapatite) na kulifanya jino kuwa imara na kutoshambuliwa na tindikali zinazotoboa meno mdomoni.”
 

Ameongeza kuwa mdomoni kuna wadudu (bakteria) ambao hutafuna mabaki ya vyakula vinavyoliwa, hasa vyakula na vinywaji vyenye sukari na kisha kutoa tindikali ambayo ndiyo sababu ya kutoboa na kuozesha meno. 

 

Dk. Nzobo, amefafanua kwamba, wadudu hao hawatoboi meno, ila huzalisha  tindikali, mara baada ya kula mabaki ya vyakula yaliyopo mdomoni hasa kwenye meno na kwenye ulimi. 


 

NIPASHE

pmbet
pmbet

Leagues standings

Tanzania Premier League
pmbet
pmbet