UTAFITI: Mtoto 'muongo' hufanikiwa zaidi maishani
Eric Buyanza
January 6, 2024
Share :
Mwanao anaongopa au kufanya michezo ya uongo?Usiogope, kwa kawaida watu waongo huwa hawaaminiki, lakini ikifika kwa watoto, yaweza kuwa sio jambo baya.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa katika Chuo Kikuu cha Toronto (University of Toronto) nchini Canada, umebaini jinsi mtoto anavyoanza mapema kuongopa ndio jinsi anavyokuwa mjanja na kuishia kuwa na mafanikio maishani.
Watafiti walichunguza watoto zaidi ya 2,000 ili kuelewa kwa nini watoto hupindisha ukweli. Katika uchunguzi huo, kila mtoto aliwekwa katika chumba chenye kamera zilizofichwa na kuwekewa mdoli nyuma yake.
Watafiti waliwaeleza watoto wasigeuke kuangalia midoli ile, kati ya watoto 10, tisa walishindwa kujizuia na kuchungulia midoli ile. Baadaye walipoulizwa kama walichungulia ile midoli, karibu watoto wote walikataa, lakini walijikuta wakitoa maelezo walipoulizwa wanahisi midoli hiyo ikoje.
Asilimia 80 ya watoto wa umri wa miaka minne huongopa.Mtafiti Mkuu, Dkt.Kang Lee anasema, asilimia 30 ya watoto wa umri wa miaka miwili huongopa, nusu ya watoto wenye umri wa miaka mitatu hutengeneza maelezo ya uongo kwa wazazi wao na mpaka asilimia 80 ya watoto wa miaka minne hutunga uongo.
Mtu akidanganya, husababisha sehemu ya ubongo inayosaidia kufikiri kufanya kazi haraka ili kuziba mapengo, hiyo humaanisha kuwa mtoto anayeongopa mapema amepiga hatua ya haraka kuweza kushawishi kwa kutumia uongo wake.
Wazazi wasistushwe na uongo wa watoto wao, wataalam wanasema, “karibu watoto wote huongopa. Wenye uelewa zaidi hufanikiwa zaidi sababu wanaweza kushawishi kwa kutetea uongo,”anasema Dkt.Lee.
Japo hatupendi kukuza taifa la waongo, ni muhimu kujua kwamba watoto wetu wanapopindisha ukweli yaweza kuwa sio jambo baya,”anaongeza.