Uturuki yasitisha biashara zote na Israel
Eric Buyanza
May 3, 2024
Share :
Uturuki imesitisha biashara zote na Israel kutokana na mashambulizi yake huko Gaza.
Wizara ya biashara ya Uturuki ilisema kuwa hatua hizo zimechukuliwa hadi pale Israel itakaporuhusu bila kuingilia kwa lolote misaada ya kibinadamu inayoingizwa Gaza.
Biashara kati ya nchi hizo mbili ilikuwa na thamani ya karibu $7bn (£5.6bn) mwaka jana.
Waziri wa mambo ya nje wa Israel alimshutumu rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kwa kuwa "dikteta".
Israel Katz alisema kwenye X kwamba Bw Erdogan "anapuuza maslahi ya watu wa Uturuki na wafanyabiashara na kupuuza makubaliano ya biashara ya kimataifa".
Aliongeza kuwa ameiagiza wizara ya mambo ya nje kutafuta njia mbadala za kufanya biashara na Uturuki, kwa kuzingatia uzalishaji wa ndani na uagizaji kutoka nchi nyingine.
Katika taarifa, Uturuki ilisema kusitishwa kwa biashara hiyo kunahusisha "bidhaa zote".
Bw Erdogan amekuwa mkosoaji mkubwa wa Israel tangu shambulio baya la Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba mwaka jana.
Mnamo Januari, alisema mashambulizi ya kijeshi ambayo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alianzisha kujibu "sio tofauti na yale aliyofanya Hitler".
Bw Netanyahu alijibu: "Erdogan, ambaye anafanya mauaji ya halaiki dhidi ya Wakurdi, ambaye anashikilia rekodi ya dunia ya kuwafunga wanahabari wanaopinga utawala wake, ndiye mtu wa mwisho anayeweza kutuhubiria maadili."
BBC