Uwanja unavyojigawa kwenye theluthi tatu kimbinu
Sisti Herman
May 6, 2024
Share :
Uwanja wa soka ambao kwa wastani hukadiriwa kuwa na urefu wa 120 m, kwenye mbinu za soka hugawanywa kwenye theluthi tatu ambazo hutumika kutafsiri mbinu za uchezaji.
Kwenye kila theluthi zamita 40 kati ya zile mita 120 za marefu ya uwanja zote huwa na majukumu ambayo wachezaji hutimiza uwanjani pale timu inaposhambulia na iinapozuia.
Hizi hapa ni theluthi 3 timu inaposhambulia (In Possession);
Theluthi ya kwanza (Build up Third)
Ni eneo ambalo lipo kwenye mita 40 za kwanza kutoka goli la timu inayomiliki mpira ambapo ndio mashambulizi ya timu yanapoanzia ambapo muunganiko ya kiuchezaji kati ya mlinda lango (golikipa) na mabeki pamoja na viungo wake hutakiwa kuwa mkubwa ili kuweza kujenga shambulizi hasa timu inayozuia inapowashiniza kufanya makosa ili kuupokonya mpira (Pressing).
Mambo muhimu kwenye theluthi hii ni;
(i) Umakini wa mlinda lango na mabeki au wote watakaoshiriki ujenzi wa shambulizi kwenye upigaji wa pasi (footwork).
(ii) Wachezaji wote kuwa kwenye eneo sahihi kulingana na muundo unaohitajika na timu (Positioning)
(iii) Uharaka, ufanisi wa pasi na mikimbio ili kutimiza dhima kuu ya theluthi hii ambayo ni uanzishwaji wa mashambulizi (Build up phase)
Theluthi ya pili (Middle Third)
Hili ni eneo ambalo huwa kwenye mita 40 za pili (kuanzia mita 50-80) ambapo hujumuisha majukumu matatu makuu kwenye hatua za ujenzi wa shambulizi;
(i) Uendelezwaji wa shambulizi lililojengwa kutoka theluthi ya kwanza ya uwanja na kuiunganisha kwenda mbele (progression)
(ii) Upenyezaji wa shambulizi katikati ya ngome ya timu inayozuia (Penetration)
(iii) Utengenezaji wa nafasi (creation)
Mambo muhimu ambayo huhitajika wachezaji kufanya kwenye theluthi hii ni;
(i) Usahihi wa wachezaji kuwa kwenye nafasi sahihi (positioning)
(ii) Kubadilishana nafasi ilikuwafungua wapinzani (Position rotation)
(iii) Muunganiko pembezoni mwa uwanja (Wide Combinations)
(iv) Mikimbio ya mtu wa tatu (third man runner) pembeni au katikati ya mistari ya uzuiaji ya wapinzani (between the lines)
(v) Ufanisi wa matendo kama upigaji wa pasi sahihi za mwisho kwa Krosi,pasi mpenyezo kwa Washambuliaji (creation)
Theluthi ya mwisho (Final Third)
Hili ni eneo ambalo lipo mita 40 za mwisho karibu na goli la mpinzani (final third) ambapo wachezaji hufanya umaliziaji wa nafasi ambazo hutengenezwa kuanzia kwenye theluthi ya pili
Mambo muhimu ambayo wachezaji huhitajika kufanya kwenye theluthi hii ni;
(i) Mikimbio sahihi na kuwa kwenye nafasi sahihi ili kuweza kupokea mipira kutoka kwa wanaotengeza nafasi za kufunga
(ii) Ufanisi wa matendo ya utengenezaji na umaliziaji wa nafasi kama mashuti, pasi
Hizi theluthi hizi 3 timu inapozuia (Out Of Possession);
Theluthi ya kwanza (Difensive Third)
Hili ni eneo ambalo huwa ndani ya mita 40 za mwanzo kutoka kwenye lango la timu inayoshambuliwa ambapo timu inayoshambulia inapokua na mpira eneo hili, timu isiyomiliki mpira huku Wachezaji wake wakiwa wengi nyuma ya mpira ili kutoruhusu timu inayoshambulia kuweza kufika langoni kwa urahisi (Low block)
Mambo muhimu ya kuzingatia kwenye uzuiaji ni;
(i) Umoja,kutoachiana nafasi kubwa kati ya mtu na mtu
(ii) Kujua wakati sahihi wa kumshinikiza mpinzani kukosea (pressing timing)
(iii) Ufanisi wa kuzuia mipira ya juu na Kusafisha inayodondoka kwa usahihi na kusafisha (Aerial and Second balls clearance)
Theluthi ya pili ya uwanja (Mid block)
Hili ni eneo ambalo lipo mita 40 za kati ya uwanja (kuanzia mita 40-80) kutoka lango la timu inayozuia ambapo huwa katikati ya uwanja
Mambo ya msingi ya kuzingatiani kutoachiana nafasi kubwa kati ya mtu na mtu, kuwasiliana pale mtego wa kuotea unapoanza kutegwa na kama utashindikana Mabeki Kuwa na uhakika wa kuweza kufanya mikimbio ya nyuma ili kuzuia hatari lakini pia mlinda lango hutakiwa kusaidia kusafisha mipira inayoelekezwa nyuma ya Mabeki wake
Theluthi ya mwisho ( High Pressing)
Hili ni eneo la kwanza la timu inayomiliki mpira ambapo timu isiyomiliki mpira hutakiwa kuzuia timu inayomiliki kutoanzisha mpira kwa uhuru(build up) na hapo hulazimika kuzuia kwa shinikizo kubwa (high Pressing) ambapo wachezaji wa timu inayozuia hushinikiza kuupokonya mpira kwa haraka kabla hujafika kwenye theluthi ya pili na ya kwanza
Mambo muhimu ya kuzingatia kwenye uzuiaji ni wachezaji timu inayozuia kuhakikisha wanakua na umoja kuweza kuwakaba wachezaji wa timu inayomiliki mpira mtu na mtu (man marking) ili kuweza kuupokonya mpira kwa haraka na kuanzisha shambulizi la kujibu (Counter attack)