Vifo vya Ebola vyafikia 220 DRC, nchi 11 zapewa tahadhari
Sisti Herman
May 27, 2026
Share :

Wakati vifo vya Ebola vikifikia 220, ikiwa ni ongezeko la watu 20 waliopoteza maisha ndani ya saa 24 zilizopita, Shirika la Afya Duniani (WHO) limetahadharisha kasi ya kuenea kwa ugonjwa huo huku Kituo cha Kukinga na Kudhibiti Magonjwa (CDC) kikisema nchi 11 zipo kwenye hatari ya maambukizi.
Nchi hizo ni Angola, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Tanzania, Zambia pamoja na Uganda ambayo maambukizi sasa yanaenea.
Onyo hilo limetolewa jana Jumatatu na Mkurugenzi Mkuu wa CDC Afrika, Dk Jean Kaseya, aliyesema hali ya sasa ni ya kutisha na inahitaji mshikamano wa haraka wa kimataifa ili kudhibiti ugonjwa huo.
“Hatuna uwezo wa kuendelea kushuhudia Waafrika wakifa. Huu ni mzigo mkubwa mno kwa bara letu,” amesema Dk Kaseya katika mkutano wa viongozi wa afya kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika uliojadili hatua za kukabili mlipuko huo.
Kwa mujibu wa taarifa za mamlaka za afya, zaidi ya watu 900 wanashukiwa kuambukizwa Ebola katika maeneo mbalimbali ya mashariki mwa DRC, huku idadi ya waliokufa ikifikia 220.
Ugonjwa huo umeenea zaidi katika jimbo la Ituri, lakini tayari kesi zimeonekana pia katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini karibu na mpaka wa Rwanda.
Shirika la Afya Duniani, WHO limesema kasi ya maambukizi imekuwa kubwa kuliko uwezo wa sasa wa kudhibiti ugonjwa huo. Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Ghebreyesus amesema timu za afya “zinaendelea kuukimbiza mlipuko” baada ya kuchelewa kugundua visa vya awali.





