Vijana kukopeshwa vifaranga vya kuku na chakula bila dhamana
Eric Buyanza
January 5, 2024
Share :
Taasisi ya EFTA inayojishughulisha na utoaji wa mikopo ya mashine na magari bila dhamana kwa wajasiriamali na wakulima nchini, imetenga Zaidi ya shilingi Bilioni 3.5 katika kipindi cha miaka mitatu ijayo kwa lengo la kuwawezesha vijana na wanawake nchini kupata mikopo ya vifaranga vya kuku, chakula Pamoja na mahitaji mengine muhimu ya ufugaji wa kuku bila dhamana.
Mpango wa mkopo wa vifaranga vya kuku kwa wakulima na hususani vijana na wanawake wasiokuwa na ajira au wanaotaka kujipatia kipato cha ziada ni wa kwanza na wa aina yake kwa taasisi ya kifedha nchini kuutoa kwa wakopaji.
EFTA imezindua mpango huu ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Rais Dr Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa akijipambanua katika kuhakikisha kuwa watanzania na hususani vijana na wanawake wanawezeshwa kiuchumi kwa kuwawezesha kupata mikopo ya aina mbalimbali ambayo itawasaidia kuanzisha shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Kwa muda sasa kundi la vijana na wanawake nchini Tanzania, ni miongoni mwa makundi ambayo yamekuwa yakitajwa kuwa na idadi kubwa ya watu wasiokuwa na ajira rasmi hatua ambayo imekuwa ikichangia kuongezeka kwa umasikini miongoni mwa kundi hili.
Kampuni ya EFTA katika kuunga mkono jitihada hizo za serikali nayo imeamua kuanzisha mpango wa majaribio wa mkopo wa kuku kwa vijana na wanawake bila dhamana. Hatua ambayo itawezesha makundi haya kushiriki moja kwa moja katika shughuli za uzalishaji kupitia uwezeshwaji wa mkopo huu bila dhamana, hatua ambayo itakuwa imeondoa ile kadhia ya vijana na wanawake kutokukopesheka katika taasisi mbalimbali za kifedha kwa kukosa dhamana.
Haya yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa EFTA, Bwana Nicomed Bohay wakati alipokuwa akiutambulisha mpango huu wa mkopo wa Kuku kwa wakazi wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini, katika hafla iliyofanyika katika kiwanda ya kuzalisha kuku cha Silverland kilichoko USA-River jijini Arusha.
Bohay amesema, mpango huu wa mkopo wa kuku kwa vijana na wanawake bila dhamana pamoja na kuunga mkono jitihada za serikali lakini unakwenda sambamba na malengo ya uanzishwaji wa taasisi yake wa kuwawezesha wajisiriamali na wakulima na hususani kutoka katika makundi hayo kujikwamua kiuchumi kupitia mikopo ya EFTA inayotolewa bila dhamana.