Vita na Iran vimekwisha - Trump
Eric Buyanza
May 2, 2026
Share :

Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza mbele ya Bunge la Marekani kuwa vita na Iran “vimekwisha,” huku akisisitiza kuwa hana nia ya kusitisha mzozo huo kwa haraka.
Rais huyo pia amejaribu kuimarisha hoja yake kwamba hahitaji idhini ya wabunge kuendelea na operesheni hiyo ya kijeshi.
Katika barua aliyowasilisha kwa viongozi wa Bunge Ijumaa, Mei mosi, wakati ukikaribia mwisho wa muda wa kuwasilisha taarifa kuhusu vita hivyo, Trump alisema hakuna mapigano yoyote yaliyotokea kati ya pande hizo mbili tangu kusitishwa kwa mapigano.
Ameiambia Congress kuwa “mapigano yaliyoanza Februari 28, 2026 yamekamilika.”
Kwa mujibu wa Sheria ya Madaraka ya Vita ya mwaka 1973 nchini Marekani, rais anaweza kutumia nguvu za kijeshi bila idhini ya Bunge kwa siku 60 pekee. Baada ya hapo, anatakiwa kusitisha operesheni, kupata idhini ya Bunge, au kuomba nyongeza ya siku 30 endapo kuna dharura ya kijeshi inayohusiana na usalama wa majeshi ya Marekani wakati wa uondoaji.
Trump pia amesema Marekani haina mpango wa kusitisha mapambano na Iran mapema, akionya kuwa kufanya hivyo kunaweza kusababisha “tatizo lilelile kujirudia baada ya miaka michache.”
Wakati huohuo, shirika la habari la IRNA liliripoti kuwa Tehran imewasilisha pendekezo jipya la mazungumzo na Marekani kupitia wapatanishi wa Pakistan, lakini Trump alilikataa haraka pendekezo hilo.
BBC





