Waandamanaji Uganda wasema wataandamana licha ya kitisho cha 'Museveni'
Eric Buyanza
July 22, 2024
Share :
Waandamanaji nchini Uganda wamesema wataendelea na mipango yao ya kufanya maadamano siku ya Jumanne, licha ya maadamano hayo kupigwa marufuku na serikali.
Tangazo hilo wamelitoa licha ya onyo kutoka kwa rais wa nchi hiyo Yoweri Museveni aliyewaambia "Wanacheza na moto".
Mapema Jumamosi, polisi nchini Uganda iliwaarifu wale wanaopanga maandamano kwamba haitayaruhusu ikitoa sababu kuwa imepata taarifa za kiintelejinsia kwamba kuna ishara za watu kutaka kutumia kutumia maandamano hayo kuleta machafuko nchini humo.
"Maandamano yanapaswa kuandaliwa chini ya ruhusa yetu kwa msingi kwamba hakuna vurugu itakayotokea au kuvuruga maisha ya raia wengine," amesema mkuu wa operesheni za polisi Frank Mwesigwa alipozungumza na shirika la habari la AFP.
Hata hivyo wale waliopanga wameapa kuendelea nayo licha ya zuio hilo la polisi.
"Hatuhitaji kibali cha polisi kufanya maandamano ya amani...Ni haki yetu ya kikatiba," amesema mmoja ya viongozi wa maandamano hayo, Louez Aloikin.