Waasi wa M23 wauteka mji wa madini wa Rubaya nchini Kongo
Eric Buyanza
May 1, 2024
Share :
Taarifa zinasema baada ya mapigano makali kati ya M23 na Jeshi la Kongo, M23 wamefaulu kuuteka mji wa Rubaya, mji muhimu wenye migodi mikubwa uliopo kwenye wilaya ya Masisi.
Milio ya mizinga ilisikika kwenye mji huo mchana kutwa siku ya jana Jumanne ambapo M23 walikuwa wakizilenga kwa makombora ngome zote za Jeshi la serikali ambalo lilishindwa kuwazuia.
Upande wao raia wamesema kuwa na wasiwasi kufuatia ukimya wa kikosi cha nchi za jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika, SADC ambacho hadi sasa kimeshindwa kukabiliana na waasi hao.
''Ni kweli kabisa mji wa Rubaya umedhibitwa na waasi wa M23 tangu hiyo jana Jumanne, kwetu ni mshangao sababu licha ya kuwepo kwa jeshi la SADC waasi wanasonga mbele na bila kuwazuiya na hata kutokabiliana nao", alisema mkazi wa Rubaya ambaye hakutaka kutajwa jina lake.
Kulingana na asasi za kiraia, kutekwa kwa mji huo ni tukio baya kwa jeshi la serikali ya Kongo ambalo halijatoa taarifa kuhusu kuchukuliwa kwa mji huo wa kimkakati.
Hadi kufikia asubuhi ya leo, mamia wa raia wa Rubaya wameendelea kukimbilia msituni huku wengine wakishindwa kutoka majumbani kufuatia milio ya risasi inayosikika kila mahali.
DW