Wachezaji na wachambuzi wazodoana mitandaoni kisa sare ya Uingereza
Sisti Herman
June 21, 2024
Share :
Baada ya kutopata matokeo yanayofurahisha kwenye michezo miwili ya mwanzo kwenye kombe la mataifa Ulaya (EURO 2024), wachezaji wa timu ya Taifa ya Uingereza wamekerwa na namna wanavyojadiliwa na wachambuzi na mashabiki kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ya nchi hiyo, ambapo mashabiki na wachambuzi wengi wamekerwa na uchaguzi wa kikosi wa kocha mkuu wa timu hiyo na kuhusisha na matokeo mabaya.
"Uingereza kwa aina ya vipaji ilivyonavyo siyo timu ya kupaki basi baada ya kuunga goli moja... namna sahihi ya sisi kuzuia ni kushambulia" aliandika Daniel Sturridge, mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo ambaye kwasasa ni mchambuzi kwenye televisheni.
Baada ya mchezo wa jana dhidi ya Denmrk uliomalizika kwa sare ya 1-1, nahodha msaidizi wa kikosi hicho Kyle Walker akihojiwa na wanahabari alisema kuwa mashabiki, wachambuzi na wadau wa soka hawapaswi kuponda bali wanapaswa kuwaunga mkono ili kutimiza malengo, kauli ambayo ilungwa mkono na aliyekuwa nahodha msaidizi wa kikosi hicho Jordan Henderson ambaye alichapisha kupitia mtandao wake wa Instagram.
Uingereza licha ya kupata sare dhidi ya Denmark na ushindi wa mbinde dhidi ya Serbia kwenye mchezo wa kwanza, wanaongoza msimamo wa kundi C wakiwa na alama 4.