Wadudu wala kiapo ofisini kwa Makonda
Eric Buyanza
May 2, 2024
Share :
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Christian Makonda amekutana na Vijana zaidi ya 223, wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali za sanaa maarufu kama ‘Wadudu’ na kuwataka kuwa Walinzi na mabalozi wazuri wa kutangaza mazuri ya Mkoa wao wa Arusha na kutojihusisha na uhalifu kwenye Jamii.
Makonda amekutana na vijana hao ofisini kwake Mjini Arusha ikiwa ni muendelezo wa kukutana na Makundi mbalimbali ya kijamii katika kuwaeleza maono yake na kuwashirikisha ili kushirikiana na Mkoa katika kujiletea maendeleo binafsi na kufanikisha malengo ya mkoa.
Katika Hatua nyingine Mkuu wa Mkoa Paul Makonda amewataka vijana hao kutumia vipaji vyao vizuri ili viwasaidia kuingiza kipato, akiwataka kumuheshimisha kama ambavyo ameonesha thamani kwao tofauti na vile ambavyo wengi walifikiri.
Mkuu wa Mkoa ametumia nafasi hiyo pia kuwataka vijana hao kumtanguliza Mungu kwenye Maisha yao, kuwa na nidhamu na kuchagua uongozi ili kufanikisha kupatiwa mahitaji ambayo tayari walikwisha kuyawasilisha kwake kwenye Kikao cha awali ambacho waliketi pamoja.
Vijana hao zaidi ya 223 wamemuahidi Mkuu wa Mkoa kutekeleza maelekezo na maagizo yake, na kuahidi kumpa ushirikiano kwenye utekelezaji wa maono yake katika Mkoa wa Arusha.