Wadukua 'Benki Kuu' na kuiba Bilioni 44 nchini Uganda
Eric Buyanza
November 29, 2024
Share :
Wadukuzi wa kimtandao wamefanikiwa kudukua mifumo ya Benki Kuu ya Uganda na kufanikiwa kuiba kiasi cha dola milioni 17 (sawa na shilingi Bilioni 44 za kitanzania), limeripoti gazeti la New Vision.
Taarifa zinasema tukio hilo lililotokea mwezi Septemba lilifanywa na kundi maarufu la udukuaji linalofahamika kwa jina la 'Waste' lenye makao yake makuu Kusini Mashariki mwa Asia.
Benki hiyo imefanikiwa kurejesha kiasi cha fedha hizo huku kiasi kingine kikielezwa kuhamishwa na wadukuaji hao na kukipeleka kwenye akaunti za Benki nchini Japan na Uingereza.
Polisi nchini humo wakishirikiana na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali wanachunguza tukio hilo ambapo taarifa za awali zinawashuku baadhi ya wafanyakazi wa Benki hiyo kuhusika kwa namna moja au nyingine.