Wafanyabiashara wadogo kunufaika na Bilioni 300
Eric Buyanza
April 10, 2024
Share :
Wafanyabiashara ndogo ndogo na za kati wapatao 2,000 watanufaika na sh. bilioni 300 ambazo zimetengwa na Benki ya Biashara Tanzania (TCB) kwa ajili ya kuwawezesha ili kuchochea ukuaji wa uchumi unaogusa watu wengi.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa TCB, Adam Mihayo, kwenye mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu utendaji wa taasisi hiyo katika kikao kilichoandaliwa na Msajili wa Hazina, jijini Dar es Salaam.
Alisema mkakati huo unaenda kutekelezwa wakati ambao benki hiyo imepata faida ya sh. bilioni 13.6 katika robo ya kwanza ya mwaka 2024 kabla ya kodi, huku faida baada ya kodi ikiwa sh. bilioni 10.7.
Mihayo alisema SME ni muhimu katika ukuzaji wa uchumi kwani zinachangia takribani asilimia 30 ya ukuaji huo.
“Tunataka kufanya uwekezaji mkubwa zaidi katika sekta ya uzalishaji, tumewaona SME watakuwa na faida kwa nchi yetu kwa sababu wanachangia asilimia 30 ya ukuaji wa uchumi,” alisema.
Alisema kuwasaidia wafanyabiashara hao kuwajengea uwezo wa mtaji kutawafanya kukua, kuajiri watu wengi zaidi na kupanua wigo wa kodi.
Kupitia fedha wajasiriamali zaidi ya 2,000 wanatarajiwa kunufaika ili kuchochea ukuaji wao kiuchumi. Aidha, alisema wamechagua kukuza SME kwa sababu zinagusa sekta nyingi nchini, akitoa mfano wa kilimo kilichoajiri watu wengi.
“Pia kuna wajasiriamali wengi ambao kupitia wadau wetu kama vile Benki ya Kilimo, inatupa chachu ya kuendelea kuwasaidia,” alisema Mihayo.