pmbet

Wahuni wavamia gereza na kuachilia huru wafungwa 4,000

Eric Buyanza

March 4, 2024
Share :

Huko nchini Haiti, magenge ya wahalifu wenye silaha wamevamia gereza kuu katika mji mkuu wa Haiti Port-au-Prince na kuwaachilia wafungwa wapatao 4,000 walikuwa wakishikiliwa kwa makosa mbalimbali.

Miongoni mwa waliozuiliwa ni wanachama wa genge walioshtakiwa kuhusiana na mauaji ya mwaka 2021 ya Rais Jovenel Moïse.

Inaarifiwa watu watano wameuwawa kwenye mkasa huo wa siku ya Jumapili. Miili mitatu ya watu waliouwawa kwa kupigwa risasi imeonekana kwenye lango la kuingia kwenye gereza hilo ambalo liliachwa wazi bila kuwepo na maafisa wa ulinzi. Miili ya watu wengine wawili imeonekana barabarani.


MAGENGE YA UHALIFU YANALENGA KUUANGUSHA UTAWALA WA ARIEL HENRY 

Kiongozi mwenye nguvu wa genge la uhalifu, Jimmy Cherisier, anayefahamika pia kwa jina la utani, Barbecue, amesema kupitia ujumbe wa video alioutuma kwenye mitandao ya kijamii kwamba, makundi yenye silaha ya Haiti yanashirikiana "kumshinikiza Waziri Mkuu Ariel Henry kuondoka madarakani."

Hadi sasa haijafahamika iwapo waziri mkuu huyo amerejea Haiti. Alikuwa ziarani nchini Kenya siku ya Ijumaa, kutafuta uungaji mkono wa kutumwa kikosi cha polisi cha kimataifa kwenda kuisaidia nchi yake.

Kenya ilikwishajitolea kuongoza kikosi hicho ambacho kiliidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Oktoba mwaka jana.

Siku ya Ijumaa, waziri mkuu Henry alitia saini mkataba na serikali ya Kenya mbele ya Rais William Ruto ili kuwezesha kutumwa kwa kikosi hicho.

Hata hivyo mpango huo unakabiliwa na kiunzi kufuatia uamuzi uliotolewa na mahakama moja nchini Kenya mwezi Januari ambao umeipiga marufuku serikali kupeleka polisi nchini Haiti.

Haiti, imetumbukia kwenye mzozo kwa miaka kadhaa sasa na mauaji ya rais ya mnamo 2021 yamechochea zaidi machafuko.

Hakuna uchaguzi uliofanyika tangu mwaka 2016 na nafasi ya wadhifa wa rais bado iko wazi.

pmbet
pmbet

Leagues standings

Tanzania Premier League
pmbet
pmbet