Waislamu wasiofunga Ramadhani Nigeria wakamatwa
Eric Buyanza
March 13, 2024
Share :
Polisi wa Kiislamu katika jimbo la kaskazini la Kano nchini Nigeria wamewakamata Waislamu 11 siku ya Jumanne ambao walionekana wakila chakula wakati wa mfungo wa Ramadhani.
Kano ina idadi kubwa ya Waislamu, ambapo mfumo wa kisheria wa Kiislamu - Sharia - unafanya kazi pamoja na sheria za kilimwengu.
Polisi wa Kiislamu, wanaojulikana sana kama Hisbah, hufanya upekuzi kwenye mikahawa na masoko kila mwaka wakati wa Ramadhani.
Wanaume 10 na mwanamke mmoja waliachiliwa baada ya kuapa kwamba hawatakosa kufunga tena kimakusudi.
"Tulipokea watu 11 siku ya Jumanne akiwemo mwanamke aliyekuwa akiuza njugu ambaye alionekana akila kutoka kwa bidhaa zake na baadhi ya watu walituarifu," msemaji wa Hisbah Lawal Fagge alisema. "Wengine 10 walikuwa wanaume na walikamatwa katika jiji lote hasa karibu na masoko ambapo shughuli nyingi hufanyika.
"Aliongeza kuwa shughuli za msako zitaendelea lakini akasema kuwa watu wasio Waislamu wamesamehewa."
''Hatuwakamata watu wasio Waislamu kwa sababu hili haliwahusu na wakati pekee ambao wanaweza kuwa na hatia ni pale tunapogundua wanapika chakula cha kuwauzia Waislamu ambacho kinatakiwa kuwa cha mfungo''.
"Kuhusu waliokamatwa alisema kuwa waliachiwa baada ya kuahidi kuanza kufunga kuanzia sasa na “kwa baadhi yao tulilazimika kuwaona ndugu au walezi wao ili kuwa na ufuatiliaji wa familia”.
Zaidi ya miongo miwili iliyopita, Sharia ilianzishwa kufanya kazi pamoja na sheria za kilimwengu katika majimbo 12 ya kaskazini mwa Nigeria ambayo yote yana Waislamu wengi.
CHANZO: BBC