Waliotimuliwa Marekani wajikuta nchini Kongo
Eric Buyanza
April 23, 2026
Share :

Kundi la wahamiaji raia wa Amerika Kusini linasema wamekwama na wana wasiwasi wa mustakabali wao mjini Kinshasa nchini DRC baada ya kufukuzwa kutoka Marekani chini ya sera tata ya uhamiaji.
Wahamiaji hao waliliambia shirika la Habari la AFP kwamba, walitumia saa 27 kusafiri huku wakiwa wamefungwa pingu, kabla ya kufika DRC nchi ambayo wengi wanasema hawakuwahi kuchagua kwenda.
Baadhi ya raia hao wanasema wanaogopa na hawawezi kuwasiliana kwa kuwa hawazungumzi Kifaransa, wengi wakisema walipewa taarifa za kupelekwa nchini humo siku moja kabla.
Kundi hilo, lenye takriban watu 15, linashikiliwa katika eneo linalolindwa karibu na uwanja wa ndege na hawaruhusiwi kutoka, baadhi wakikiri kupokea kiasi kidogo cha fedha na wengine kuugua.
DRC ni miongoni mwa mataifa ya Afrika ikiwemo Eswatini, Rwanda, Ghana, Cameroon na Equatorial Guinea ambayo yaliingia makubaliano na Marekani kupokea wahamiaji wanaofukuzwa na Washington.
RFI





