Walioua mamba wetu walifuata utaratibu - TAWA
Sisti Herman
January 2, 2024
Share :
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) imesema imekamilisha uchunguzi uliokuwa unafanywa ili kuona kama kuna ukiukwaji wa sheria za uwindaji baada ya kuonekana kwa video ya Mwindaji wa Marekani Josh Bowmer akifurahia kuwinda mamba mkubwa nchini Tanzania na kuleta taharuki, ambapo uchunguzi umeonesha mamba huyo aliwindwa kitalu cha Lake Rukwa GR kwa kibali halali, ada na tozo zote za uwindaji zililipwa na hakuna utaratibu uliokiukwa.
Taarifa iliyotolewa leo January 02,2024 na TAWA imesema “Kwa mujibu wa taratibu za mkataba wa kimataifa wa CITES, Tanzania imeruhusiwa kuwinda mamba wasiozidi 1,600 kwa mwaka, mpaka sasa mamba 39 tu kati ya 1,600 wamewindwa kutoka kwenye mgawo (quota) wa Taifa wa mwaka 2023, mamba anayeonekana kwenye picha jongefu (video clip) iliyosambaa aliwindwa katika kitalu cha Lake Rukwa GR kwa kibali halali namba MP-0001792 kilichoanza tarehe 12/08/2023 hadi 09/09/2023”
“Mamba huyo alikuwa na urefu wa futi 16.2 sawa na sentimita 493.8 ikiwa ni juu ya kiwango cha chini cha urefu wa sentimita 300 unaohitajika kwa mujibu wa sheria, aidha kwa mujibu wa takwimu za taasisi ya Marekani (Safari Club International- SCI), mamba mrefu zaidi duniani aliwindwa chini Ethiopia mwaka 2005 (futi 18.7 sawa na sentimita 561)”
“Vilevile, kumbukumbu zinaonesha, uwindaji huu ulisimamiwa na Askari kutoka TAWA na Mwindaji bingwa kutoka kwenye kampuni iliyopewa kibali kwa mujibu wa sheria, ada na tozo zote zinazohusiana na uwindaji wa mamba zililipwa kwa kuzingatia sheria na kanuni zinazosimamia uwindaji hapa nchini, hivyo taratibu zote hizi za kisheria zilizingatiwa na hakuna utaratibu uliokiukwa.
“TAWA inawahakikishia Wananchi kuwa uwindaji wa wanyamapori nchini unazingatia Sheria na taratibu za ndani ya Nchi na zile za kimataifa na Mamlaka inawatoa hofu kuwa taratibu hizi zinasimamiwa ipasavyo na pale panapotokea ukiukwaii hatua stahiki huchukuliwa kwa mujibu wa sheria” ——— ameeleza Afisa Habari wa TAWA Beatus Maganja.