Wamiliki wa mabasi ya Sauli na New Force watakiwa kujieleza
Eric Buyanza
April 3, 2024
Share :
Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), imewataka wamiliki wa mabasi ya Sauli na New Force yaliyosababisha ajali Machi 28, 2024 wilayani Kibaha, Mkoani Pwani na kusababisha vifo vya watu wawili kutoa maelezo kwa maandishi kabla ya kuchukuliwa hatua za kiudhibiti.
LATRA imesema, kwa mujibu wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, ajali hiyo imetokana na uzembe wa dereva wa basi namba T 668 DTF Scania mali ya Mwalabhila Sauli kutaka kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari, huku madhara ya ajali hiyo yakisababishwa na uzembe wa dereva wa basi namba T 175 DZU linalomilikiwa na kampuni ya New Force kushindwa kuacha umbali wa gari lililokuwa mbele yake kama inavyopaswa.
Pia, kulingana na taarifa za Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS), tarehe ya tukio magari namba T 175 DZU na T 668 DTF yalianza safari kutoka Dar es salam kwa pamoja saa 8:44 usiku, ambapo kwa mujibu wa leseni walizopewa, mabasi hayo yalipaswa kuanza safari saa 9:00 na saa 10:30 alfajiri.