Wamuua Andrea kisha mwili wake wakaufukia ndani ya nyumba
Eric Buyanza
April 4, 2024
Share :
Mwanaume wa miaka 77 aliyefahamika kwa jina la Andrea Mayunga, mkazi wa Kijiji cha Mwamashimba Kata ya Lyamidati wilayani Shinyanga, ameuawa na kisha mwili wake kufukiwa ndani ya nyumba.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, Janeth Magomi, amebainisha hayo jana wakati akizungumza na Waandishi wa Habari, na kwamba tukio hilo limetokea Machi 29, mwaka huu.
Amesema iligundulika kuwa Mayunga alitoweka nyumbani katika mazingira ya kutatanisha na baada ya taarifa hizo kulifikia Jeshi la Polisi lilifanya ufuatiliaji na kufanikiwa kuupata mwili wa marehemu ukiwa umefukiwa ndani ya nyumba inayodaiwa kumilikiwa na Hang Toshaga.
Amesema baada ya kufanya uchunguzi wa kitabibu iligundulika kuwa marehemu ameuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani, na kisha watuhumiwa kuamua kuufukia mwili wake ndani ya nyumba ili kuficha ushahidi.
“Chanzo cha tukio hili ni kulipiza kisasi cha ugomvi uliokuwepo kati ya marehemu na familia ya mtuhumiwa, na tunawashikilia watu watatu ambao ni Mussa Samweli, Njile Nkilijiwa, Masele Bubinza ambaye ni mganga wa kienyeji, na taratibu za kipelelezi zikikamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani,” amesema Magomi.