Wanafunzi 3 wafariki dunia, baada ya lori kupoteza muelekeo
Eric Buyanza
October 31, 2026
Share :

Wanafunzi watatu wa kidato cha tatu wa Shule ya Sekondari Mringa, iliyopo wilayani Arumeru, wamefariki dunia papo hapo baada ya kugongwa na gari katika barabara ya Bypass iliyopo Kijiji cha Kiushini.
Ajali hiyo imetokea jana Oktoba 30, 2026 saa 10 jioni katika barabara hiyo iliyopo Kata ya Olorien, ambapo lori hilo inaelezwa liliacha njia na kugonga gari ndogo aina ya Toyota Rumion kisha kuwagonga watembea kwa miguu hao watatu (wanafunzi) ambao walifariki papohapo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo, imewataja waliofariki kuwa ni Bianka Juma, Catherine Pius na Jesca Sabore, ambao wote walikuwa wanafunzi wa kidato cha tatu katika shule hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa Dereva lori hilo lililokuwa likiendeshwa na Abdul Seleman, mkazi wa Arusha, ambaye alikuwa anayapita magari mengine bila kuchukua tahadhari.
"Chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa lori ambaye alikuwa anayapita magari mengine bila kuchukua tahadhari hali iliyosababisha kwenda kugonga gari dogo lililokuwa limepaki pembeni ya barabara na kukosa uelekeo," ameeleza Kamanda.





