Wanafunzi waaandamana na kuchoma majengo ya serikali
Eric Buyanza
July 19, 2024
Share :
Maandamano ya wanafunzi yanayoendelea nchini Bangladesh yamesababisha uharibifu mkubwa wa majengo ya serikali na kuzimwa kwa mtandao wa intaneti kote nchini humo.
Watu wasiopungua 39 wamepoteza maisha, huku idadi ya vifo ikitarajiwa kuongezeka zaidi kufuatia ripoti za makabiliano kwenye nusu ya wilaya 64 za nchi hiyo.
DW imeripoti kuwa Taarifa iliyotolewa na polisi imesema kuwa waandamanaji wamechoma na kuharibu ofisi nyingi za polisi na serikali.
Miongoni mwa ofisi hizo, ni makao makuu ya shirika la utangazaji la Bangladesh, Televisheni ya Dhaka, ambayo hadi sasa bado haiko hewani baada ya mamia ya wanafunzi waliojawa na hasira kuvamia jumba hilo na kuchoma moto jengo.
Wanafunzi hao wanataka kukomeshwa kwa mfumo wa ajira serikalini ambao wanasema unayapendelea makundii maalum ikiwemo watoto wa vigogo.