Wanafunzi wanaongoza kuoga dawa za kuvutia wapenzi
Eric Buyanza
June 11, 2024
Share :
Waganga wa jadi katika Kata ya Kagongwa, Halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga wamesema wamekuwa wakipokea idadi kubwa ya wanafunzi wanaotaka dawa za mvuto wa mapenzi maarufu kama samba, ili wapate wanaume wenye fedha.
Wamesema kinachowachochea wanafunzi hao kutafuta dawa hiyo ni kutokana na baadhi ya wazazi na walezi wao kuendekeza mila hizo kwa kutaka kupata mali mapema, hali inayosababisha wanafunzi wengi kukatisha masomo na kujiingiza katika vitendo vya ngono wakiwa na umri mdogo na kupata mimba pamoja na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).
Walieleza hayo juzi wakati wa kikao kilichowakutanisha viongozi wa madhehebu ya dini, waganga wa jadi, wazee, waendesha bodaboda na vijana.
Akizungumzia adha hiyo katika kikao hicho, mmoja wa waganga wa jadi, Jongela Heneriko, alisema wanafunzi wanaongoza kuwatembelea kwa kutaka kuogeshwa dawa za mvuto wa mapenzi, kwa lengo la kutaka wanaume wenye uwezo wa kifedha ili kukidhi mahitaji yao ya shule.
Alisema kitendo cha wanafunzi kuja kuomba dawa hizo kinasababishwa na wazazi wenye tamaa ya kupata mali, hususani kipindi cha mavuno ambapo ndoa nyingi hufungwa.
Alisema kumekuwa na utamaduni usiokuwa na tija wa kutafuta dawa za mvuto, ili kuwavutia wanaume ambao wameuza mazao na kupata fedha.
NIPASHE