Wanajeshi Kongo wahukumiwa kifo kwa kukimbia vita
Eric Buyanza
May 4, 2024
Share :
Mahakama ya kijeshi katika mji wa Goma huko Kivu Kaskazini Mashariki mwa Congo imewahukumu kifo maafisa nane wa jeshi la Congo, FARDC kwa tuhuma za kukimbia vita na kutoheshimu sheria za kijeshi.
Miongoni mwao ni Kanali Shamba mkuu wa kikosi cha makomandoo pamoja na msaidizi wake.
Mwendesha mashtaka amesema makamanda hao walishindwa kuwajibika kwenye uwanja wa mapambano karibu na mji wa Sake wilayani Masisi eneo lililo magharibi mwa mji wa Goma ambako M23 wanaendelea kudhibiti vijiji.
Wakili wa makamanda hao Bwito Jean Richard wa Jeshi linaloitii serikali amesema mahakama imefanya makosa kutoa adhabu ya kifo kwa wanajeshi hao ambao walikuwa wamejitolea kulipigania taifa.
Hata hivyo amekata rufaa na kuionya Mahakama kuwa makini kwa kuwa hatua za mahakama zinaweza kupelekea wanajeshi wengi kugoma kwenda vitani.
Lakini baadhi ya wachambuzi wamesema hatua hii itawazuia wanajeshi kukimbia mapigano kila mara na kuwaacha waasi wakichukua vijiji.
Katika hukumu hiyo wanajeshi watatu, kapteni mmoja na maluteni wawili waliachiliwa huru na mahakama kwa madai ya kutokuwa na hatia.
Makamanda hao walipewa adhabu ya kifo kwa mujibu wa sheria za nchi hiyo.|
VOA