Wanaume wahonga makahaba magunia ya mpunga, wake zao walia njaa
Eric Buyanza
April 26, 2024
Share :
Baadhi ya wakazi wa Kata ya Mwamala Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, wameiomba serikali kuzinusuru familia zao kufa kwa njaa kutokana na waume zao kuhonga makahaba magunia ya mpunga katika kipindi cha mavuno na kusababisha wao na watoto kukosa chakula.
Mkazi wa Kijiji cha Mwamala 'B', Salima Sosoma amesema katika maeneo ya vijijini kuna idadi kubwa ya wanawake kutoka mjini wanaojifanya wanauza vileo (pombe) huku wakiwa wanauza miili yao kwa ujira wa kubadilisha kuanzia debe moja la mpunga hadi gunia kwa vijana na waume zao hali inayosababisha familia zao kukosa chakula.
“Kama unavyojua sie wanawake wa Kisukuma hatuna sauti mbele za wanaume zetu na ukijifanya mjuaji unaadhibiwa mbele ya watoto, tunaiomba serikali iingilie kati na kuwaondoa madada poa ambao wengi wao wanafukuzwa mjini na kukimbilia vijijini kutapeli mazao yao,” amedai.
Ofisa Kilimo wa Kata hiyo, West Mwanda, amesema amekuwa akikemea tabia hiyo mara kwa mara hasa anapowatembelea wakulima.
Amewataka wakulima kuacha tabia ya kuwapa mpunga wanawake wanaouza miili yao na wale wanaouza kwa lengo la kujipatia fedha kwa ajili ya familia zao wauze kichache na kuacha kingine kwa matumizi ya nyumbani.
NIPASHE