Wanawake watishia kutembea uchi, ikiwa Waziri hatarudishwa kazini
Eric Buyanza
July 24, 2024
Share :
Katika hali ya kushangaza baadhi ya wanawake wakazi wa Mlima Kenya wametoa wito wa kurudishwa kazini kwa aliyekuwa Waziri wa Utumishi wa Umma Moses Kuria, ikiwa ni siku chache baada ya Rais Ruto kuvunja Baraza lake la mawaziri.
Wakiongea na waandishi wa habari, Pierra Muthoni, almaarufu kwa jina la Mama Dan, alisema wanawake wa Nyakinyua Ndumo, Ol Kalou, hawakufurahishwa na kufutwa kazi kwa Moses Kuria.
Kwa mujibu wa Mama Dan aliyekuwa akiongea kwa niaba ya wenzake, Kuria alisaidia vijana wengi katika eneo hilo wakati alipokuwa Waziri, kwani kupitia michezo, vijana wengi wameacha maovu na kujikita kwenye michezo.
"Mimi Pierra Muthoni AKA Mama Dan, na sisi ni Nyakinyua Ndumo kutoka Olkalou huko Nyandarua. Hatufurahii Moses Kuria kuachishwa kazi kwa sababu alipokuwa waziri alifanya kazi nzuri sana. Alileta pamoja vijana kupitia mashindano ya soka na vijana walikuwa wameacha kunywa pombe na kuvuta bangi," alisema.
Wanawake hao wakamsihi Rais Ruto amrudishe Kuria kwenye kazi yake ya awali kwani ni mchapakazi, na ikiwa hatafanya hivyo basi watavua nguo na kutembea uchi barabarani.
"Kwa hiyo tunakuomba rais. Tunakusihi... Sisi kama wanawake Nyakinyua Ndumo tunataka kurejeshwa kwa Kuria kwenye kazi yake ya awali, ikiwa hutaki tuvue nguo na kutembea uchi, Moses Kuria lazima arudishwe kazini," Muthoni aliongeza.
TUKO