Wanigeria washangazwa 'Aki' kuoa mke mwingine kimyakimya
Eric Buyanza
July 20, 2024
Share :
Kutoka kwenye kiwanda cha filamu za Kinigeria, muigizaji mkongwe Chinedu Ikedieze, anayefahamika na wabongo wengi kwa jina la 'Aki', amewashangaza wapenzi wa kazi zake nchini humo baada ya hivi majuzi kujulikana ya kwamba alioa mke wa pili kimyakimya bila wengi kufahamu.
Hilo lilijulikana baada ya muigizaji huyo kubandika chapisho kwenye mtandao wake wa Instagram akisherehekea siku ya kumbukizi ya kuzaliwa ya mwanamke aliyemtambulisha kama Stephanie Promise Ikedieze...chapisho ambalo lilikuwa na maneno matamu ya kimahaba.
Ndani ya chapisho hilo 'Aki' alielezea jinsi anavyompenda na kumshurukuru mungu kuwajalia watoto wawili wa kike na hivi karibuni mungu kuwaongezea mtoto mwingine wa kiume.
Hata hivyo, Stephanie Promise sio mwanamke ambaye Chinedu (Aki) alimuoa mwaka 2011 kwa ndoa ya kimila iliyozua gumzo kubwa nchini Nigeria.
Muigizaji huyo alifunga ndoa na Nneoma Nwaijah mwaka wa 2011, lakini kulingana na chapisho lake la juzi, inaonekana wawili hao hawako pamoja tena.