Wapinzani Uganda waungana kumuangusha Museveni
Eric Buyanza
January 18, 2024
Share :
Viongozi wa vyama vikuu vya upinzani Uganda, akiwemo Robert Kyagulanyi (Bobi Wine) na mwanasiasa maarufu nchini Uganda Dkt Kizza Besigye wametangaza kuungana kwa ajili ya kumuangusha Rais Yoweri Museveni katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2026.
Meya wa mji wa Kampala Erias Lukwago ambaye pia ni rais wa chama cha FDC ameelezea kuwa muungano huo ni mwendelezo wa harakati zao za kuikomboa Uganda kutoka katika utawala wa kiimla wa Rais Museveni.
"Taifa hili ni kubwa kuliko kujenga vyama vyetu vya siasa. Katika nchi ambayo hata chama cha siasa hakiwezi kuendesha shughuli zake hatuwezi kujivunia kuwa vyama vya siasa, kwa hiyo sote ni watumwa na tunapozidi kupigana miongoni mwetu, tunaendeleza utawala wa Museveni," alisema Rais wa chama cha NUP Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine.