"Wasanii rudisheni mikopo, ili wengine wakope" - Mh Hamis Mwinjuma
Eric Buyanza
July 24, 2024
Share :
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma @mwanafa ,ameuagiza Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania ukutane na kuzungumza na baadhi ya wasanii waliokopa fedha awali kupitia mfuko huo na kushindwa kurejesha kwa wakati kabla ya kuanzishwa kwa utararibu mpya wa kutumia benki kukopesha wasanii ili kuangalia namna bora ambayo wanufaika hao watarejesha mikopo hiyo akisisitiza kuwa hakuna mkopo utakaofutwa.
Mhe. Mwinjuma ametoa agizo hilo Julai 23 2024 Jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na wanufaika wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa ambapo pia ameelekeza itafutwe namna bora ambayo itasaidia mikopo yote kurejeshwa.
"Kila fedha iliyotolewa na Mhe. Rais kwa ajili ya kukopesha wasanii lazima irudi, mtu yeyote, aliyekopeshwa fedha anatakiwa kurejesha ili wasanii wengine wanufaike, tutakachofanya ni kuangalia utaratibu rahisi utakaowezesha baadhi ya walioshindwa kurejesha kwa wakati warejeshe"
"Namuagiza Mtendaji Mkuu wa mfuko akae nanyi, naomba mtoe ushirikiano, muangalie namna ambayo itawawezesha kurejesha mikopo yenu, mathalani kupunguza kiwango cha marejesho hii yote ni kuhakikisha fedha yote inarejeshwa" amesisitiza Mhe. Mwinjuma.