Watafiti waanza uchimbaji ilipo safina ya Nuhu
Sisti Herman
September 25, 2026
Share :

Watafiti nchini Uturuki wameanza kuchimba na kuchunguza kwa kina kiakiolojia eneo la kihistoria linaloaminika kuwa ndipo ilipotia nanga, Safina ya Nuhu.
Utafiti na uchimbaji huo unafanyika katika Wilaya ya Doğubayazıt mkoani Ağrı, mashariki mwa Uturuki.
Eneo hili lina umbo la kipekee linaloaminika kufanana na meli kubwa, ambalo liligunduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1959 na mhandisi wa ramani wa jeshi la Uturuki aitwaye Kapteni İlhan Durupınar.
Muundo wa Durupinar, ulioko karibu na Mlima Ararat nchini Uturuki, umekuwa ukihusishwa na safina ya Nuhu, chombo kikubwa cha majini kilichojengwa na Nuhu kwa maagizo ya Mungu ili kuokoa familia yake na wanyama wakati wa gharika kuu, kulingana na kitabu cha Mwanzo kwenye Biblia.





