Watangazaji waliomhoji Dogo Paten wafungiwa na Bodi ya Ithibati.
Joyce Shedrack
July 18, 2025
Share :
Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari imewapiga marufuku kuendelea na kazi watangazaji Crispin Mgenge, Perfect Crispin na Iddy Bakari wa Kipindi cha Genge kinachorushwa na Mjini Fm hadi pale watakapotimiza matakwa ya sheria ikiwa ni pamoja na kuwa na sifa za kielimu na kuzingatia maadili ya taaluma ya habari nchini.
Hatua ya Bodi hiyo inakuja baada ya kufanya nao mahojiano na tathmini ya kitaaluma mara baada ya kufanya kipindi na Msanii Dogo Paten, mahojiano yaliyoibua taharuki kwenye mitandao ya kijamii kutokana na maudhui ya Mahojiano yao na msanii huyo wa Muziki wa Singeli suala ambalo liliilazimu Bodi kufanya tathmini ya maudhui hayo.
"Watangazaji hao hawajasajiliwa na kupewa ithibati na bodi hivyo wanafanya kazi za kihabari kinyume na sheria ya huduma za habari, watangazaji hao walikiuka haki ya faragha na kutweza utu wa mhojiwa kwa kumlazimisha kutoa taarifa binafsi bila ridhaa yake kinyume na kanuni za mawasiliano ya kielektroniki na posta na pia watangazaji hao walitumia lugha ya kumshushia hadhi mhojiwa kinyume cha kanuni za mawasiliano." Imesema taarifa ya bodi ya ithibati.
Kulingana na taarifa kwa vyombo vya habari, Watangazaji hao wamefungiwa kujihusisha na masuala ya kihabari kuanzia Julai 18, 2025 mpaka hapo watakapotimiza matakwa ya kisheria ikiwa ni pamoja na kuwa na sifa za kielimu na kuzingatia maadili ya taaluma ya habari