Watatu wa Familia moja wauawa na kuchomwa moto Dodoma
Sisti Herman
September 17, 2024
Share :
Watu watatu wa Familia moja Wakazi wa Mtaa wa Segu Juu Jijini Dodoma wamefariki dunia kwa kile kinachodaiwa kupigwa na kuchomwa moto na Watu wasiojulikana usiku wa kuamkia leo September 17,2024 huku Mama wa Familia hiyo akijeruhiwa vibaya na Mtoto mmoja wa Familia akinusurika.
Waliofariki ni Watoto wawili na Mdada wa kazi za ndani huku Mama wa Watoto akiwa amejeruhiwa maeneo mbalimbali ya mwili wake na kupelekwa Hospitali kwa matibabu ambapo Baba wa Famili hiyo ambaye ni Mwalimu Mkoani Singida amefika Dodoma na kuonekana akiwa analia kwa uchungu katika eneo la tukio akihoji kilichoipata Familia yake.
Majirani na Mwenyekiti wa Mtaa huo wamedai baada ya Mtoto aliyenusurika katika tukio hilo kufungua mlango walikuta damu zimetapakaa kwenye nguo za marehemu hao ambao wamepigwa na kuchomwa moto huku Mama yao ambaye alikuwa chumba cha pili akikutwa na majeraha.
Shuhuda mmoja amesema “Kale Katoto nilikuta kameshatoka na ndiko kalikofungua milango, milango ilikuwa imefungwa kwa ndani kwa jinsi nilivyomuona Mtoto ni kama alikuwa amepigwa, uso umevimba, mashavu yamejaa, rasta zinadamu, Mwenyekiti aliposema tumbebe nguo zote zina damu, Mtoto alikuwa anaambiwa fungua akawa anasema naogopa, wakamlazimisha hadi akafungua”
“Watu hawa wamepigwa na hata moto ni kama ulitaka tu kupoteza ushahidi waonekana wameungua, inaonekana kuna Mtu alikuja akataka kuchukua kitu chake akaona pamefungwa ndiye alitoa taarifa, huu moto sio wa bahati mbaya ni tukio limetengenezwa, ukiingia sebuleni umaona ni damu Mtu ameburuzwa, walioungua sielewi kama walipigwa wakachomwa moto maana chumba kilichoungua ni kimoja vingine havijaungua, Mama yao ana hali mbaya sana amekimbizwa Hospitali”